Jumatatu 18 Agosti 2025 - 16:08
Somo la Akhlaq | Kwa Nini Uislamu Unalipa Umuhimu wa Pekee Swala la kuunga udugu?

Hawza/ Uislamu umetilia mkazo mkubwa juu ya sila rahm (kuunga udugu), si tu kwa maana ya kuunganisha uhusiano wa kifamilia, bali pia kwa maana ya kuyalinda mahusiano muhimu mawili ya kimaumbile ya mwanadamu: tumbo la mama na tumbo la dunia, matika mtazamo huu, mwenendo na lishe ya wazazi hata kabla ya kuzaliwa mtoto huchangia kwa kiasi kikubwa katika furaha au maangamizi ya maisha yake ya baadaye, kutilia mkazo sila rahm ni kuheshimu muungano huu wa kimwili, kisaikolojia na kiroho tangu mwanzo wa uhai hadi mwisho wa maisha ya duniani.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Marehemu Ayatollah Hasan Zadeh Amoli – mjuzi wa maadili na mwanafalsafa mashuhuri wa ulimwengu wa Kishia – katika moja ya masomo yake ya akhlaq alizungumzia mada ya “Falsafa ya kuunga udugu”.

Sheria ya Kiislamu imeeleza kwamba mwanadamu hupitia katika “matumbo” mawili, tumbo la kwanza ni tumbo la mama, ambalo ni chimbuko la uhai wa kidunia na mahali pa malezi ya awali, tumbo la pili ni tumbo la dunia, ambalo ndani yake sasa hivi sote tunaishi. Kama vile tulivyohitaji uangalizi na malezi katika tumbo la kwanza, vivyo hivyo tunahitaji uangalizi na uongofu tukiwa katika tumbo la pili "dunia" hii ndiyo sababu tumesisitiziwa kutekeleza kuunga udugu na kuepuka kuukata.

Dhanna ya kuunga udugu na kuukata ina upeo mpana sana, moja ya vipengele vyake muhimu ni kuhusiana na tumbo la kwanza, yaani tumbo la mama, wazazi wanapaswa kulinda na kuendeleza muungano huu wa kimaumbile katika kipindi cha ujauzito na kujiepusha na jambo lolote litakaloathiri muungano huo, huu si muungano wa kifamilia pekee, bali unahusu pia nyanja za kimwili, kisaikolojia na kiroho.

Mfano wake ni kwamba mtoto anapokuwa tumboni, tusisahau kuwa tumbo la mama si eneo la kimaumbile tu kwa ukuaji, bali pia ni msingi wa hatima ya furaha au maangamizi ya baadaye, kulingana na ubora wa lishe, mwenendo na maadili ya wazazi wake.

Mtoto tumboni ni sehemu ya mwili wa mama; kupitia kitovu, hupokea kila kitu kutoka kwa mama – ikiwa ni pamoja na afya na usafi wa chakula, ikiwa chakula cha mama kimetokana na mali haramu, basi baba kwa hakika amefanya kitendo cha kuvunja udugu kwa sababu amempa mtoto chakula kisicho halali, na hivyo kuharibu msingi wa muungano wake wa kimaumbile, athari za chakula hicho katika roho na nafsi ya mtoto zinaweza kuwa na madhara yasiyorekebishika.

Kwa maana hiyo, kama chakula cha mama ni cha haramu au kichafu, basi mtoto naye huathirika moja kwa moja, na uchafu huo huacha athari za kina za kiroho, ndiyo maana imeelezwa: “Mzazi anatakiwa kuwa makini asije akamfanya mtoto awe mwovu akiwa bado tumboni kutokana na lishe na mwenendo wake.”

Katika hadithi ya kusisimua imesemwa: “Mtu muovu huwa muovu tangu tumboni mwa mama; na mtu mwema huwa ni mwema tangia huko,” Kwa maneno mengine, hatima ya mwanadamu huamuliwa tangu hatua za awali za ujauzito, ikiwa wazazi hawatakuwa makini katika mwenendo wao, maneno yao, na hasa katika riziki wanazopata, basi mtoto ambaye angeweza kuwa miongoni mwa mashahidi na wema anaweza kubadilika na kuwa mwovu.

Kinyume chake, iwapo wazazi watakuwa waangalifu kwa nia safi na matendo yenye uhalali, basi mtoto tumboni ataandaliwa maisha yenye baraka na furaha.

Kwa mtazamo huu, dunia ni tumbo letu la pili, na tumbo la mama ni tumbo la kwanza, kama vile tunavyotakiwa kulinda muungano na uhusiano katika maisha ya duniani, ndivyo pia tunavyotakiwa kulinda uhusiano wa kiroho katika tumbo la mama, kuukata udugu si tu kutokutembeleana ndugu, bali ni kila kitendo au mwenendo unaoharibu muungano huu muhimu wa kimaumbile na kiroho.

Kwa hivyo, majukumu ya wazazi katika kipindi cha ujauzito si ya kimwili pekee, bali ni ya kimaamuzi kuhusu mustakabali wa mtoto, baba anatakiwa kutafakari ni vipi atamuingiza mtoto wake katika tumbo la dunia:

Kwa usafi na uhalali, au kwa uchafu na maangamizi.

Hivyo ndivyo falsafa ya kuunga udugu inavyotufunza: kuuenzi muungano wa asili na kiroho tangu mwanzo wa uhai hadi mwisho wa maisha ya duniani.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha